Kipindupindu (Cholera)

Kipindupindu ni ugonjwa wa kuambukiza ambao unahusiana na kuharisha maji maji.

Usipo tibiwa mara moja na kwa haraka, mwathirika anaweza kufa ndani ya masaa machache.

Sababu na Maambukizi

Ugonjwa wa Kipindupindu unasababishwa na bakteria anayeitwa Vibrio cholerae.

Kwa kawaida hupatikana katika chakula au maji machafu na kinyesi kutoka mtu aliye na maambukizi. Kwa hiyo, huambukizwa kwa njia zifuatazo:

 • Usambazaji wa maji machafu
 • Barafu iliyotengenezwa kwa maji machafu
 • Vyakula na vinywaji vilivyo na bakteria
 • Mboga zilizopandwa kwenye maji taka
 • Samaki na dagaa waliovuliwa kwenye maji machafu

Hatua za Ugonjwa

Vimelea vinapoingia mwilini, vinatoa sumu yake ndani ya matumbo. Sumu hiyo, husababisha kuwashwa kwa matumbo na matukio mbalimbali kama kuharisha na kutapika ghafla. Hali hiyo hupelekea upungufu wa maji mwilini na hatimaye inaweza kusababisha kifo kwa mwathirika wa kipindupindu.

Makundi yanayoweza kuambukizwa kwa haraka:

 1. Wasafiri
 2. Sehemu zenye mikusanyiko ya watu wanaokula kama hotelini, harusini na kadhalika.
 3. Wafanyakazi wa afya
 4. Waandaji wa vyakula mtaani (Mama nitilie).
 5. Wakazi wa makazi duni
 6. Wavuvi
 7. Watoto

Dalili za kipindupindu

Dalili za ugonjwa wa kipindupindu zinaweza kuonekana ndani ya masaa machache au siku tano baada ya maumbukizi.

Dalili hizo ni:

 • Kuharisha maji maji (maji yanayofanana na maji ya mchele)
 • Kutapika
 • Mapigo ya moyo kwenda haraka
 • Upungufu wa maji mwilini unaosababisha kusinyaa kwa ngozi, ukavu wa mdomo, koo, na pua
 • Kushuka kwa shinikizo la damu
 • Maumivu ya misuli
 • Kiu mara kwa mara

Mazingira Hatarishi ya ugonjwa wa kipindupindu

Maambukizi ya kipindupindu ni kawaida kwa makazi ya mijini na vijijini au katika mazingira yenye upungufu wa maji safi. Yafuatayo ni baadhi ya mambo hatarishi:

 • Ukosefu wa vyoo bora au matumizi wa vyoo duni inachangia maambukizi ya kipindupindu.
 • Kambi zilizo na msongamano mkubwa zinaweza kuongeza hatari ya maambukizi ya kipindupindu
 • Ukosefu wa maji safi na salama pamoja na kutozingatia njia za usafi kama kunawa mikono na maandalizi ya vyakula
 • Mabadiliko ya hali ya hewa, kwa mfano, Msimu wa kiangazi unaoendana na uhaba wa maji na msimu wa mvua nyingi unaoambatana na mafuriko
 • Upungufu wa Kinga mwilini kwa watoto, watu wenye utapiamlo, wazee, akina mama wajawazito, VVU / UKIMWI miongoni mwa wengine.
 • Ukosefu wa kutambua ugonjwa mapema na matibabu sahihi
 • Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kuwa watu wenye kundi la damu O wana hatari Zaidi kuathirika kwa sababu zisizojulikana.

Utambuzi (Jinsi ya kutambua ugonjwa wakipindupindu)

Uchunguzi unaofanywa ili kuthibitisha maambukizi ya kipindupindu ni pamoja na:

 • Kupima Damu
 • Kupima Kinyesi

Tiba

Lengo la matibabu ni kurejesha maji na chumvi zilipotezwa wakati wa kuharisha.

Kuharisha na kupoteza maji inaweza kukithiri, na kuwa vigumu kurejesha kiwango cha maji mwilini.

Kulingana na hali ya mgonjwa, anaweza akapewa maji kupitia mdomoni au kwenye mishipa (IV). Dawa za Antibiotics zinaweza kupunguza muda wa ugonjwa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) wamegundua njia nafuu na rahisi ambayo husaidia kurejesha maji mwilini.

Jinsi ya Kuzuia ugonjwa wa kipindupindu

Njia zifuatazo husaidia kuzuia ugonjwa wa kipindupindu:

 • Kuzingatia njia sahihi za usafi.
 • Kunawa mikono kwa sabuni mara kwa mara, hasa baada ya kutumia choo na kabla ya kushika chakula.
 • Matumizi ya vyoo wakati wote.
 • Tumia maji safi na salama yaliyo chemshwa, ama yaliyo changanywa na kemikali ya kuua wadudu, au maji ya chupa kwa matumizi yafuatayo:
  • Kunywa
  • Kuandaa chakula au vinywaji
  • Kutengeneza barafu
  • Kusafisha meno
  • Kuosha uso wako na mikono
  • Kuosha vyombo
  • Kuosha matunda na mboga

Usitumie / usile chakula kibichi, kama vile:

 • Matunda na mboga ambazo hazijamenywa
 • Maziwa ambayo haijachemshwa
 • Nyama na Samaki ambao hawajapikwa

BUY TRAVEL COVER

FIND A SPECIALIST

BMI CALCULATOR

REQUEST FOR A QUOTE

medical-insurance-kenyabackpain-medical-insurance-kenya